Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Oktoba 08, 2022 Local time: 01:59

Baraza la mahakama kuamua adhabu ya mlipua bomu Boston


Mchoro wa picha ya Dzhokhar Tsarnaev (C) akiwa na wanasheria Miriam Conrad (L) na Judy Clarke (R) wakati kesi ikiendelea.

Baada ya kumkuta na hatia katika shambulizi la bomu katika mbio ndefu za Boston Marathon mwaka 2013 Dzhokhar Tsarnaev baraza la mahakama litachukua siku chache za mapumziko kabla ya kuamua iwapo impe hukumu ya adhabu ya kifo au kifungo cha maisha jela.

Baada ya siku mbili za mashauriano marefu na makini katika mahakama ya serikali kuu baraza la mahakama hapo Jumatano lilimkuta na hatia Tsarnaev mwenye umri wa miaka 21 kwa mashtaka yote 30 anayokabiliana nayo ikiwemo 17 ambayo yana uwezekano wa kupatiwa adhabu ya kifo. Hatua ya hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kuanza katika chumba hicho hicho cha mahakama wiki ijayo mjini Boston nchini Marekani.

Baraza la mahakama litatakiwa kupiga kura ya pamoja ili kutoa hukumu ya kifo kwa Tsarnaev.

Tamerlan Tsarnaev (L) na Dzhokhar Tsarnaev
Tamerlan Tsarnaev (L) na Dzhokhar Tsarnaev

Wanasheria wake walikiri kutoka mwanzo wa kesi kwamba Dzhokhar alihusika kupanga kulipua mabomu yaliyotengenezwa kienyeji kwa kutumia sufuria maalumu karibu na mstari wa kumaliza mbio zinazofanyika kila mwaka za Boston Marathon na kusababisha vifo vya watu watatu akiwemo mvulana mwenye umri wa miaka minane pamoja na kuwajeruhi 264 wengine huku watu 17 wengine wakipoteza sehemu za viungo vya mwili na wengine wengi kubaki na ulemavu wa maisha kutokana na majeraha waliyoyapata.

Lakini upande wa utetezi ulisihi kwamba kaka yake aliyekuwa na mtazamo mkali Tamerlan Tsarnaev mwenye umri wa miaka 26 alikuwa mhusika mkuu kwenye shambulizi hilo. Wakili wa utetezi Judy Clarke ambaye amefanikiwa kuwaepusha na adhabu ya kifo washukiwa wengine walioshtakiwa kwa mauaji Marekani aliliambia baraza la mahakama kwenye taarifa yake ya kufunga “kama sio Tamerlan, tukio hilo lisingetokea”.

Tamerlan Tsarnaev aliuwawa siku kadhaa baada ya milipuko ya April 15 mwaka 2013 wakati Dzhokhar alipomgonga kwa gari kwa bahati mbaya wakati ndugu hao wawili walipokuwa wanajaribu kuwakimbia polisi waliokuwa wakiwasaka kwenye maeneo yote ya Boston. Walimfyatulia risasi na kumuuwa polisi mmoja wa chuo kikuu wakati wakijaribu kuwakimbia maafisa.

Boti aliyojificha Dzhokhar huko Boston
Boti aliyojificha Dzhokhar huko Boston

Dzhokhar aliishi Marekani kwa muda wa muongo mmoja kabla ya tukio hilo la ufyatuaji mabomu na baadaye alipatikana akiwa amejificha ndani ya boti moja iliyoegeshwa nyuma ya nyumba kwenye eneo la wazi katika kiunga kimoja huko Boston.

Waendesha mashtaka walisema Dzhokhar aliandika maandishi yasiyosomeka vyema kuhusu shambulizi hilo ndani ya ukuta wa boti hiyo kwamba ndugu hao walijaribu kulipiza kisasi mashambulizi ya waislam yanayofanywa na Marekani katika vita vya Marekani nchini Iraq na Afghanistan.

XS
SM
MD
LG