Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:48

Ban Ki Moon azungumza na rais Kenyatta kuhusu kambi ya Daadab


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimpigia simu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano kumshinikiza asiwaondoe wakimbizi kutoka kambi ya Daadab.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimpigia simu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano kumshinikiza asiwaondoe wakimbizi kutoka kambi ya Daadab.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, siku ya Jumatano alimpigia simu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kutoa shinikizo kwamba nchi hiyo isiwahamishe wakimbizi kutoka kambi ya Daadab kama ilivyopangwa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Bwana Ban Jumatano usiku ilisema kwamba mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alitoa wito kwa Kenyatta kurejerea tena mkataba uliotiwa saini na wadau watatu mnamo mwaka wa 2014 kuhusiana na swala hilo.

Wadau hao ni Kenya, Somalia na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu.

Ban aliitaka Kenya kutafuta mikakati itakayowawezesha wakimbizi hao kurudi makwao kwa hiari na wala sio kwa kulazimishwa.

Ban alimhakikishia Kenyatta kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuiunga Kenya mkono na kupongeza ukarimu wake kwa kuendelea kutoa hifadhi kwa wakimbizi wanaotoroka hali mbaya ya kisiasa na mizozo mingine nchini mwao.

Wiki mbili zilizopita, Kenya ilitangaza kwamba itafunga kambi ya wakimbizi ya Daadab kwa kile ilichokiita "sababu za kiusalama na kiuchumi."

Hata hivyo, serikali za nchi zingine na mashirika mengi yanayoshughulikia maswala ya haki za binadamu yameiomba Kenya kubatilisha uamuzi wake.

Ingawa Umoja wa Mataifa ulikuwa umetoa taarifa kuikosoa Kenya kwa msimamo wake, hii ni mara ya kwanza kwa Bwana Ban kuzungumzia swala hilo moja kwa moja.

Hadi tulipokuwa tukiandaa ripoti hii, Sauti ya Amerika haikuwa imepata msimamo wa rais Kenyatta kufuatia mazungumzo hayo.

Daadab ndiyo kambi kubwa zaidi ulimwenguni ikiwa na wakimbizi zaidi ya laki tatu na nusu.

XS
SM
MD
LG