Viongozi wa Umoja wa Afrika walifungua rasmi mkutano wa siku mbili Jumapili mjini Addis Ababa na kumchagua mwenyekiti mpya kuongoza shirika hilo. Rais wa Benin Thomas Yayi Boni alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa mwaka mmoja na hivyo kuchukua hatamu za uongozi kutoka kwa rais wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alikuwa wa kwanza kutoa hotuba katika makao makuu ya Umoja wa Afrika yaliyogharamiwa na kujengwa na China, mshirika mkubwa wa kibiashara kwa bara la Afrika. Bwana Ban aliwaambia viongozi wa Umoja wa Afrika kuwa chaguzi 25 zijazo za marais, wabunge na mabaraza barani humo mwaka huu sharti zifanyike kwa kuzingatia haki na usawa. Alizisihi serikali za Sudan na Sudan Kusini kutanzua tofauti za mafuta yanayopatikana kwenye mpaka baina yao. Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa pia alisema Somalia ni taifa lililogubikwa na matatizo mengi ya kijamii lakini taifa ambalo linaweza kujikwamua na kuwa na maisha mazuri ya baadaye. Viongozi hao wa Umoja wa Afrika wanatazamiwa kuzungumzia mzozo wa Somalia na pia mzozo unaoendela baina ya Sudan na Sudan Kusini.
AU yafungua mkutano Addis Ababa

Rais wa Benin Thomas Yayi Boni akabidhiwa uongozi wa AU