Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 22, 2023 Local time: 17:51

Askofu Tanzania apinga vikwazo dhidi ya viongozi wa dini


Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (K.K.K.T) nchini Tanzania amesema kuwa suala la amani siyo la wanasiasa peke yao na kuwa linapaswa kuhubiriwa na wadau wote ikiwa ni pamoja na taasisi za dini.

Askofu Benson Bagonza, amesema kwamba huwezi kusema viongozi wa dini wasishiriki katika siasa wakati kila kitu wanachofanya kinatokana na siasa.

Amefafanua kuwa :“...Hili shati nililovaa bei inapangwa na wanasiasa, kukubali kununua nimeshashiriki siasa, ni kitu kisichowezekana unakula, unalala, unaamka hii ni siasa, kwa hiyo tunaishi katika nchi ya siasa."

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania Askofu Bagonza aliyasema hayo Ijumaa Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ambao uliwahusisha pia viongozi wa dini.

"Viongozi wa dini wana wajibu wa kushauri na kuonya pale wanapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani, hivyo kujitenganisha na siasa haitawezekana," alisema Askofu.

“Hatuwezi kukaa katika nchi kama tupo peponi, yapo matukio ya uvunjifu wa amani ambayo yanatokea ni lazima tukemee," alisisitiza.

“Kanisa lina nguvu karibu miaka 2,000, hivi vyama hakuna kilichofika hata miaka mia, maana hii habari ya viongozi wa dini kuongelea siasa imekuwepo kwa miaka 2,000 sasa,” alisema Askofu Bagonza.

Alisema maendeleo bila siasa ni kujidanganya, “ilani zinatungwa na wanasiasa, huwezi kutenganisha siasa na taasisi za dini," aliongeza.

XS
SM
MD
LG