Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 23, 2024 Local time: 02:38

Askari -Tanzania adaiwa kumuuwa raia aliyekuwa chini ya ulinzi


Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, kaka wa marehemu Chacha Heche
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, kaka wa marehemu Chacha Heche

Polisi wilaya ya Tarime Rorya, Mkoa wa Mara nchini Tanzania wanamshikilia afisa polisi kwa madai ya kuwa amemchoma kisu na kumuuwa raia Chacha Heche (24), mdogo wake Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche siku ya Ijumaa.

Kamanda Henry Mwaibambe, amethibitisha Jumamosi kuuwawa kwa Chacha na kueleza kuwa marehemu alikuwa na mgogoro na mmoja wa askari waliokuwa wamekwenda kumkamata.

“Marehemu alikuwa na mgogoro na mmoja ya askari waliokuwa wamemkamata na kufikia hatua ya kutaka kupigana ndipo askari aliposhindwa kujizuia na kumchoma kisu,” amesema kamanda huyo.

Mbunge Heche katika ukurasa wake wa Facebook ameandika, “Watu hawako salama tena mikononi mwa polisi. Mdogo wangu Suguta amekamatwa na polisi jana usiku na ameuawa na polisi kwa kuchomwa kisu. Najisikia maumivu mno, hii sio nchi ambayo tunaitaka. Najiuliza maswali mengi ni kwa vipi mtu amefungwa pingu anachomwa kisu tena na polisi.”

Naye, kaka wa marehemu Heche Suguta, ambaye ni Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), aliliambia gazeti la Nipashe kuwa taarifa za msiba huo walizipokea jana.

“Msiba upo nyumbani kwangu Salasala, Dar es Salaam, nilivyosimuliwa ni kwamba alikuwa kwenye baa iliyopo Tarime Rorya, polisi walikwenda kumkamata sababu za kumkamata hatujaelezwa, ila nimeambiwa mmoja wa askari waliokwenda kumkamata walikuwa na ugomvi naye,” alisema.

Hata hivyo, alisema kitendo hicho kilichofanywa na askari huyo sio kizuri ni bora angempeleka kituoni kuliko kumuua.

Polisi imesema tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati Chacha akipelekwa kituo cha polisi, limeripoti gazeti la Nipashe nchini Tanzania.

Alisema wakati wakielekea kituoni ulitokea mzozo kati ya askari na Chacha na kufikia hatua ya kutaka kupigana.

“Askari mwenzake aliyekuwa katika tukio hilo aliingilia kuamua ndipo ilipotokea askari huyu alipomchoma kisu cha mgongoni mtuhumiwa huyu na kumsababishia kifo,” alisema.

Alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi jana mchana mbele ya ndugu zake na umekutwa na jeraha la kisu.

Kamanda Mwaibambe alisema, mtuhumiwa huyo alikuwa hajavalishwa pingu na haijafahamika nini waliambiana mpaka ikatokea hali hiyo.

Hata hivyo, alisema kwa wakati huo hali katika kituo cha polisi imetulia baada ya awali wananchi kufurika kulalamikia mauaji hayo.

“Nawaomba wananchi kutochukulia tukio hili kisiasa, hili ni sawa na matukio mengine ya mauaji ingawa siyo jambo zuri lililotendeka, nimeshaongea na ndugu wa familia kuwaeleza jinsi tukio lilivyokuwa,” alisema.

Jana baada ya tukio hilo, wananchi walifurika kituo cha polisi cha Sirari, hali iliyosababisha polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

XS
SM
MD
LG