Steve Jobs mwanzilishi mwenza na mkuu wa kampuni ya Apple, kampuni ya vifaa maarufu duniani vya komputa, iPhones, iPads na iPods amejiuzulu kutoka wadhifa wake.
Katika barua aliyotolewa Jumatano, Jobs aliiambia bodi ya wakurugenzi wa Apple na jamii ya Apple, kuwa hawezi tena kufanya kazi zake na matarajio kama mkurugenzia mkuu mtendaji wa kampuni hiyo.
Jobs amekuwa akiuguwa ugonjwa wa saratani ya bandama na alibadilishwa ini lake. Amekuwa kwenye likizo ya afya tangu mwezi Januari.
Habari hiyo ilipelekea mara moja kushuka kwa bei ya hisa kwa zaidi ya asilimia tano baada ya saa za kawaida za biashara.
Apple ilisema katika taarifa yake kwamba Jobs aliiokoa Apple kutokana na mtazamo wa kipekee na uongozi stadi. Kampuni ilisema Jobs amechaguliwa kama mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na katika jukumu hilo ataendelea kuchangia kwa kutoa mitazamo ya kipekee, ubunifu na kuhamasisha.
Taarifa ilisema Tim Cook atachukua nafasi hiyo kama mkurugenzi mkuu kutokana na pendekezo la Jobs. Kabla ya hapo Cook alikuwa afisa mkuu wa utawala wa kampuni. Bodi ya Apple ilisema Cook amefanya kazi kwa miaka 13 na Apple na alidhihirisha ustadi wake na kuchukua maamuzi thabiti katika kila kitu alichokifanya.
Apple hivi sasa ni moja kati ya makampuni maarufu na yenye thamani kubwa duniani, lakini katika miaka ya 1990, kampuni hii ilikuwa nusura kufilisika. Mapato yake yalipatikana wakati ilipobadili mwelekeo kutoka utengenezaji wa kompyuta za binafsi na kuwa kampuni ya kutengeneza simu za kisasa iPhone na kompyuta ya teknohama ya iPad.