Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 21:57

Annan kuongoza mazungumzo ya kisiasa nchini Syria


Kofi Annan, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na mjumbe maalumu katika kusuluhisha mzozo wa kisiasa nchini Syria, Machi 11, 2012
Kofi Annan, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na mjumbe maalumu katika kusuluhisha mzozo wa kisiasa nchini Syria, Machi 11, 2012

Kofi Annan amesema mzozo wa Syria unabidi kushughulikiwa kwa tahadhari ili kuepuka makosa yatakayopelekea vurugu kubwa kwa kanda nzima

Mjumbe maalum wa umoja wa nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alitoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumaliza mvutano wao na kuishinikiza Syria kukomesha ukandamizaji wake dhidi ya upinzani unaosababisha umwagaji damu.

Akitoa maelezo mafupi kutoka Geneva siku ya Ijumaa, mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa, alisema anapeleka ujumbe Damascus wiki ijayo kujadili mpango wa kuwapeleka wafuatiliaji wa kimataifa. Wanadiplomasia wanasema Bwana Annan alikua analiarifu baraza hilo, karibu wiki moja tu baada ya mikutano na Rais wa Syria, Bashar al-Assad mjini Damuscus.

Wanadiplomasia wa nchi za magharibi wanasema wana matumaini mazungumzo ya bwana Annan yataongeza juhudi za kupitisha azimio la Umoja wa Mataifa linalolaani ukandamizaji wa bwana Assad dhidi ya wapinzani na kusababisha umwagikaji damu. Russia na China zimepiga kura ya turufu mara mbili dhidi ya azimio hilo linaloilaani Syria.

Baada ya kutoa maelezo mafupi, bwana Annan aliwaambia waandishi wa habari kuwa msukosuko wa kisiasa nchini Syria unahitaji kushughulikiwa kwa tahadhari, ili kuepuka makosa yeyote ambayo yatapelekea vurugu kubwa zaidi jambo litakalo athiri kanda zima.

Vyombo vya habari vya serikali ya Syria vilitoa taarifa Ijumaa kabla ya maelezo ya bwana Annan, vikisema serikali inaahidi kushirikiana na mjumbe maalum ili kutafuta suluhisho la kisiasa kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo. Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje nchini humo kwa mara nyingine iliwalaumu magaidi na wageni kuingilia kati kwa sehemu kubwa ya ghasia zinazosababisha maafa nchini humo.

Waandamanaji wanaoipinga serikali ya Syria waliandamana tena Ijumaa, siku moja baada ya serikali nchini humo kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuzuka ghasia za kisiasa.

Wanaharakati wanasema maelfu ya waandamanaji waliomba jeshi la kimataifa kuingilia kati wakati walipoandamana katika miji kadhaa ikiwemo Aleppo na Homs. Pia kulikuwepo na ripoti za kufyatuliwa risasi.

XS
SM
MD
LG