Maelfu ya wafuasi wa chama tawala cha Afrika kusini cha ANC wamekuwa wakisherehekea ushindi wa chama chao mwishoni mwa wiki katika mji wa Johannesburg licha ya kwamba chama hicho kilipunguza idadi ya viti vyake katika bunge la taifa kwa kushinda asilimia 57 za kura. Hali ambayo wachambuzi walisema inabidi chama hicho kikongwe cha Afrika kutafakari mikakati na majukumu yake ya siku zijazo hasa kutokana na kuongezeka kwa ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani.
Idadi ya wapiga kura waliojitokeza wiki iliyopita katika uchaguzi mkuu ulioisha nchini Afrika Kusini ilikuwa ndogo na wachambuzi walisema hii ni ishara kuwa chama tawala cha African National Congress- ANC kinahitaji kujiangalia tena na kulenga kutatua matatizo ya wananchi wa Afrika Kusini.
"Ni mchanganyiko wa ujumbe, lakini tukiangalia kwa usawa kwa haki ANC imepata asilimia 58 baada ya miaka 25 madarakani, marais watano na uchaguzi wa sita. Sio mbaya sana lakini pengine ingekuwa mbaya zaidi. Lakini kwa ujumla ninadhani ukweli ni kwamba chama cha upinzani EFF kimeongeza karibu nusu ya kura zake na ni chama ambacho wapiga kura wake wengi wametoka ANC, kwa maoni yangu ninadhani huo ndio ujumbe muhimu kwa ANC, kwamba inahitaji kujipanga upya, kujitathmini na kushughulikia maslahi na mahitaji ya wa Afrika Kusini wote kwa ujumla".Otieno alisema kitu cha kuogopesha hapa ni idadi ndogo ya vijana waliojitokeza kupiga kura.
Chama cha ANC hakijawahi kushinda chini ya asilimia 60 ya kura zake katika uchaguzi mkuu. Ushindi wa ANC umekipa chama hicho viti vya kutosha bungeni kumpa Rais Cyril Ramaphosa miaka mitano mingine ofisini lakini bila nguvu za kutosha za kupambana na upinzani ambao unapinga sera zake za kufufua uchumi.
Viti vya ANC bungeni vimepungua kutoka 249 mpaka 230. Chama cha upinzani cha Democratic Alliance nacho kimeshuhudia viti vyake vikipungua kutoka 89 mpaka 84 huku chama kingine cha upinzani EFF kinachoongozwa na Julius Malema kikiongeza viti vyake kutoka 19 mpaka 44.