Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 20:02

Marekani haipendelei Aristide kurudi Haiti


Rais wa zamani wa Haiti, Jean-Bertrand Aristide
Rais wa zamani wa Haiti, Jean-Bertrand Aristide

Serikali ya Marekani Alhamisi imeeleza upinzani wake na uwezekano wa kurejea Haiti kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Jean-Bertrand Aristide. Maafisa wa Marekani wamesema kuwa wakati bado kuna kumbukumbu ya kurejea kwa dikteta wa zamani wa nchi hiyo Jean-Claude Duvalier, kurejea kwa mtu mwingine mwenye utata ni kitu cha mwisho ambacho Haiti inahitaji.

Maafisa wa Marekani wameweka wazi wasiwasi wao kwamba kurejea kwa Jean-Claude Duvalier, na tetesi za kurejea kwa bw. Aristide, kunatishia kuvuruga jitihada za Haiti kukarabati nchi baada ya tetemeko la ardhi na kutatua utata uliotokea katika utaratibu wa uchaguzi.

Bw. Aristide ambaye alikuwa Raisi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Haiti, amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu akimbie mwaka 2004 kufuatia upinzani mkubwa dhidi ya utawala wake.

Kufuatia kurudi bila ya kutazamiwa kwa bw. Duvalier, Jumapili iliyopita, bw. Aristide ametangaza kwamba naye anataka kurejea nyumbani kuisaidia nchi yake, na amesema anaamini wenyeji wake, Afrika Kusini watawezesha hilo.

Maafisa wa Marekani wamekataa kutoa maoni kama wanaishinikiza Afrika Kusini kumzuia bw. Aristide asirejee Haiti. Lakini akizungumza na waandishi wa habari wa kimataifa mjini Washington, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, P.J Crowley, amesema kwamba ukichukulia matatizo ambayo nchi hiyo inakabiliana nayo, basi jambo la mwisho ambalo halihitajiki ni kurejea kwa viongozi wa zamani na kufufuka migogoro iliyopita.

P.J Crowley amesema “Haiti inahangaika kushughulikia utata wa utaratibu wa uchaguzi uliopo sasa. Na hatuamini kuwa matukio yeyote kufanywa na mtu yeyote kwa wakati huu yatakayoweza kuleta mgawanyiko kwa jamii ya wa-Haiti, yataisaidia Haiti kusonga mbele, hasa kwa sababu watu wa Haiti wanahitaji kuchomoza kwa serikali mpya ambayo wataiamini, na kuwa na uhakika nayo kuwa itaiongoza Haiti kuelekea kwenye mafanikio”

Uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana ulionekana kwa sehemu kubwa uligubikwa na wizi wa kura na kasoro chungu nzima hata kusababisha ghasia za wananchi. Duru ya pili ya uchaguzi ambayo ilipangwa kufanyika Jumapili iliyopita iliahirishwa, wakati Umoja wa Mataifa ya Amerika-OAS, unachunguza shutuma za kasoro zilizotokea katika uchaguzi wa awali.

Alhamisi katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu juhudi za kuijenga upya Haiti kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka mmoja uliopita, Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema kuendelea kwa misaada ya kimataifa huko Haiti kunahitaji utaratibu wa uchaguzi unaoaminika.Pia alizungumzia juu ya kile alichokiita rekodi mbaya ya ukiukwaji wa haki za binadamu na rushwa, vinavyomkabili Rais wa zamani Duvalier, na kuelezea wasiwasi wake kuhusu madhara yasiyotabirika katika hali ya kisiasa yanayoweza kutokana na kurejea kwake.

Kaimu msemaji msaidizi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mark Toner, amesema umakini unapaswa kuelekezwa kwenye mustakbali wa Haiti, pamoja na kuisaidia kukamilisha utaratibu wake wa uchaguzi, na kuongeza kuwa kiongozi aliye uhamishoni Aristide, sio jambo linalohitajika kukamilisha mambo haya.


XS
SM
MD
LG