Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 18:43

Al-Shabab yadai kuhusika na mashambulizi ya Kampala


Polisi wa Uganda wakichunguza mripuko wa bomu kwenye mgahawa wa Ethiopian Village mjini Kampala abaada ya mripuko wa mabomu Jumapili usiku.

Kundi lenye uhusiano na Al-Qaida huko Somalia, al-Shabab limedai kuhusika na mabomu mawili ya Jumapili mjini Kampala, Uganda. Idadi ya waliofariki katika mashambulizi hayo imefikia zaidi ya 70.

Msemaji wa kundi la Al-Shabab Ali Mohamud Rage, maarufu kwa jina la Ali Dheere, akizungumza na waandishi habari mjini Mogadishu Jumatatu alisema mashambulio ya mabomu mawili yaliyotokea Kampala ni ulipizaji kisasi dhidi ya Uganda kwa kutowaondowa wanajeshi wake kutoka Somalia.

Uganda ina zaidi ya nusu ya wanajeshi 6,100 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika AMISOM, huko Somalia. Jukumu lake ni kuilinda serikali ya mpito inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kutokana na mashambulio ya waasi, na kimekua kikipigana takriban kila siku na wapiganaji wa al-Shabab huko Mogadishu tangu kikosi cha kwanza cha Uganda kuwasili 2007.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda alilaani shambulio hilo alipotembelea maeneo yaliyoharibiwa na mabomu na kuapa kwamba watawasaka wahusika. Viongozi wa nchi mbali mbali za dunia wamelaani mashambulio hayo na kuahidi kuisaidia serikali ya Uganda. Msemaji wa White House amesema rais Obama alizungumza na rais Museveni na kuahidi msaada wa Marekani.

Maafisa wa usalama huko Kampala wanasema idadi ya walofariki imeongezeka na kufikia 74, wengi wa walofariki ni wale waliokua wakitizama fainali ya kombe la dunia katika klabu ya mpira wa rugby.

XS
SM
MD
LG