Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 31, 2023 Local time: 18:39

Afrika kusini yapeleka wanajeshi Congo


Wanajeshi wa Congo wakisubiri kupelekwa kwenye mstari wa mbele wa mapigano huko mashariki ya nchi
Mkuu wa jeshi nchini Afrika kusini alisema wanajeshi wa Afrika kusini ambao wanapatiwa mafunzo kwa ajili ya kazi za kijeshi za Umoja wa Mataifa nchini Congo watakuwa wamejiandaa vyema hata kama jeshi la Afrika kusini kwa jumla halina vifaa vya kutosha na fedha.

Luteni Jenerali V.R Masondo pia aliviambia vyombo vya habari kwamba vikosi vya Afrika kusini vinapatiwa msaada wa mafunzo na wanajeshi ambao walishiriki katika tume ya ulinzi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati-C.A.R. Mwezi machi waasi huko waliwauwa wanajeshi wa Afrika kusini 14 wakati walipoukamata mji mkuu Bangui na kumuondoa madarakani Rais Francois Bozize.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kikosi kipya cha kuingilia kati huko Congo kikiwa na mamlaka ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya makundi ya waasi ili kusaidia kuleta amani katika sehemu za mashariki zenye utajiri mkubwa wa madini nchini humo, eneo hilo limekumbwa na mapigano tangu kumalizika kwa mauaji ya halaiki mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda. Jeshi la Congo lilisema watu 32 waliuwawa katika mapigano kati ya wanajeshi wa Congo na wanamgambo ambao walishambulia mji wa kaskazini wa Goma, siku ya Jumatano.

Masondo alisema bajeti ya kiasi cha dola bilioni 1.1 kwa jeshi la Afrika kusini haitoshi kukidhi mahitaji yake ambayo yanajumuisha kukarabati vifaa vya zamani na majengo yaliyo katika hali mbaya na majukumu kama vile operesheni za kigeni, doria za mpakani, kulinda hospitali wakati wa migomo ya wafanyakazi, kuandikisha wahamiaji na kuwasaidia polisi.

Changamoto za fedha zinafanya iwe vigumu “kufanya kila kitu ambacho tunatakiwa kukifanya” alisema Masondo. Lakini alikiri kuwa kuna “mahitaji ya lazima” kwa serikali ya Afrika kusini kuelekeza rasilimali kwenye program za kijamii na kiuchumi katika nchi yenye idadi kubwa ya watu wasio na ajira na mwanya mkubwa kati ya matajiri na maskini.

Alisema wanajeshi wanaoelekea Congo “wamejiandaa vyema” licha ya mapungufu katika jeshi.

Umoja wa Mataifa ulisema kiasi cha wanajeshi 100 wa Tanzania waliwasili huko mashariki mwa Congo Mei 11, hatua ya kwanza katika kukusanya kikosi kipya. Wanajeshi wanaosalia watawasili kwa awamu, lakini hakuna tarehe ya mwisho iliyotajwa kwa wanajeshi hao. Malawi pia imeahidi kupeleka wanajeshi japokuwa baadhi ya wataalamu wa masuala ya kijeshi wanahoji kama kuwepo kwa wanajeshi elfu kadhaa wanatosha kurejesha usalama huko.
XS
SM
MD
LG