Jeshi la angani la Nigeria, Jumanne limedai kwamba limemjeruhi vibaya kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, na viongozi wengine wa ngazi za juu wa kundi hilo, katika mashambulizi yaliyolenga makao makuu ya kundi hilo la kigaidi.
Sani Usman, msemaji wa kikosi cha angani cha Nigeria, alisema kupitia taarifa yake alisema kwamba Shekau alijeruhiwa vibaya kwenye bega baada ya ndege za serikali kurusha bomu kwenye makao yao yaliyo katika msitu wa Sambisa mnamo siku ya Ijumaa.
Kulingana na Usman, viongozi wengine wa Boko Haram waliouawa katika shambulizi hilo ni pamoja na Abbakar Mubi, Malam Nuhu na Malam Hamman, huku wengine kadhaa wakithibitishwa kujeruhiwa.
Siku za nyuma Nigeria ilishawahi kudai kumuua Shekau, lakini madai hayo yakatiliwa shaka pale video iliyomuonyesha mtu aliyejitambulisha kama Shekau ilijitokeza.
Taarifa ya Usman haikutoa habari zaidi kuhusu kifo cha kiongozi huyo wa Boko Haram, wala kundi hilo kusema lolote kuhusiana na madai hayo.