Benki kuu ya Dunia imetangaza mpango utakaogharimu dola milioni 200 kusaidia kupambana na malaria katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.
Msaada huo mpya wa fedha utatumiwa kwa ajili ya kusambaza na kutoa vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa kusaidia kuwalinda watu kutokana na ugonjwa huo unaouwa watu wengi katika bara hilo.
Juhudi za kuzuia ugonjwa wa malaria zitalenga nchi zinazoathirika sana zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ethiopia, Ghana, Kenya, Msumbiji, Sierra Leone na Zambia.
Malaria inauwa takribani watu milioni moja kila mwaka na wengi wao kutoka bara la Afrika. Wanaoathirika zaidi ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Rais wa Benki kuu ya Dunia Robert Zoellick, anasema msaada huo mpya utasambaza vyandarua milioni 25. Anasema vyandarua ni muhimu katika juhudi dhidi ya malaria na shirika hilo lina nia ya dhati kuhakikisha wote walio hatarini na ugonjwa huo wanalindwa.
Vyandarua vingine milioni 25 vitahitajika ili kuwafikia wale wote walio kwenye hatari ya malaria duniani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ameweka lengo la kutokomeza vifo vya malaria ifikapo mwaka 2015.