Marekani imeitaka serikali ya Sudan kuondoa haraka masharti kwa vyama vya kisiasa kabla ya uchaguzi uliopangwa kuanza siku ya Jumapili.
<!-- IMAGE --> Msemaji mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, P.J Crowley, alielezea wasi wasi huo Jumatatu kuhusu kile alichokiita maendeleo ya mashaka nchini Sudan ikiwemo masharti makali ya uhuru wa kisiasa ambayo yameleta khofu kuhusu harakati za kisiasa nchini humo. Crowley alisema Marekani itaunga mkono kucheleweshwa kidogo kwa uchaguzi wa urais, wabunge na upigaji kura wa majimbo kama hilo litasaidia kutatua matatizo kuhusu harakati za uchaguzi.Lakini serikali ya Khartoum tayari imeshakataa wito wa upinzani wa kuchelewesha uchaguzi ikisisitiza kwamba ni uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Sudan tangu ule wa mwaka 1986 na utafanyika kama ulivyopangwa.
Upigaji kura unaotarajiwa kuanza Jumapili unatarajiwa kuendelea kwa siku 3. Uchaguzi huo ni sehemu ya mkataba wa amani nchini Sudan wa mwaka 2005 ambao ulimaliza mapigano kati ya maeneo ka kaskazini na kusini.