<!-- IMAGE -->
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma pamoja na viongozi wa upinzani nchini humo wametoa wito wa utulivu kufuatia mauwaji ya kiongozi wa makaburu wanaotaka kujitenga. Mauwaji hayo yanaainika yametokea kufuatia ugomvi juu ya mshahara, lakini viongozi wa upinzani wameonya kwamba taarifa za uchochezi kutoka kwa viongozi wa chama tawala cha ANC zinaweza kuzidisha hali ya mvutano nchini humo.
Rais Zuma alilaani mauwaji ya kiongozi wa wazungu wenye itikadi kali Eugene Terre'Blanche, aliyeuliwa Jumamosi kwenye shamba lake kaskazini magharibi ya Johannesburg.
Katika taarifa yake Zuma alitoa wito wa kuwepo utulivu na kuwahimiza wananchi kustahmiliana na kutoruhusu tukio hilo kuzusha chuki za kikabila.
Polisi wanasema Terre'Blanche aliyekua na umri wa miaka 69, alipigwa hadi kufariki kufuatia ugomvi wa mshahara na wafanyakazi wake wawili. Wanasema watu hao wawili wamekamatwa.
Hapo 1973 Terre'Blanche alianzisha vuguvugu la makaburu Afrikaaner Resistance Movement, AWB katika lengo la kuendeleza utawala wa wazungu chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini.
AWB ilipinga majadiliano yaliyopelekea utawala wa waafrika walowengi na kuongoza mashambulizi ya mabomu katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa kihistoria wa 1994 nchini humo. Terre'Blanche alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu mwaka 2001 baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia na kumuua kikatili mwafrika katika kituo cha kuuza mafuta.
Katika miaka ya karibuni kiongozi huyo wa makaburu alipigania kuundwa kwa jamhuri ya wazungu pekee ya Afrika Kusini. Waziri wa polisi wa Afrika Kusini Nathi Mthethwa alikutana Jumapili na familia ya kiongozi huyo mkulima na kujaribu kukana baadhi ya ripoti yanayo husisha mauwaji hayo na itikadi kali za kibaguzi za Terr'Blanche.