Jarida la Forbes limetoa orodha yake ya mwaka ya watu matajiri duniani Jumatano, na kwa mara ya pili tu tangu mwaka 1995, mwanzilishi wa kampuni ya kompyuta ya Microsoft hajashika nafasi ya kwanza.
Taji la tajiri mkubwa kuliko wote duniani mwaka huu limekwenda kwa raia wa Mexico, Carlos Slim, mmiliki wa kampuni ya mawasiliano ikiwa na thamani ya jumla ya dolla billioni 53 na nusu. Slim ambaye kampuni yake kuu America Movil inamiliki rasilimali kadha za makampuni ya mawasiliano, ni mtu wa kwanza ambaye si Mmarekani kutangazwa kuwa tajiri mkubwa kuliko wote tangu mwaka 1994, ambapo Mjapan Yoshiaki Tsutsumi alishika nafasi hiyo.
Lakini utajiri wa Slim unampita Bill Gates kwa dolla millioni 500 tu na kumfanya Mmarekani huyo ashikilie nafasi ya pili akiwa na utajiri wenye thamani ya dolla billioni 53. Warren Buffet, Mmarekani mwingine ameshika nafasi ya tatu mwaka huu, akiwa na utajiri wa dolla billioni 47.
Kulingana na gazeti hilo Gates angeweza kushika nafasi ya kwanza mwaka huu pia kama asingetoa fedha zake nyingi katika misaada mbali mbali duniani. Thamani ya utajiri wake ingekuwa dolla billioni 80.