Wafanyakazi wa uwokozi waliendelea kwa siku ya pili kuwatafuta watu ambao huwenda walinusurika kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotikisa eneo la kati la Chile mapema Jumamosi asubuhi. Na Rais Michelle Bachelet akitembelea maeneo yaliyoathirika alilipatia jeshi udhibiti kamili wa usalama wa mji uloharibiwa zaidi wa Concepcion.
Bi Bachelet alitoa wito wa msaada wa kimataifa wakati mitetemeko zaidi ya 100 ilitokea siku ya pili baada ya tetemeko kubwa kabisa kurikodiwa katika kipindi cha karne moja. Rais alitoa pia wito kwa sekta za umaa na kibinafsi huko Chile kusaidia na juhudi za kuikarabati nchi wakati misaada inamiminika kutoka kila pembe ya dunia.Tetemeko hilo lililokua na nguvu za 8.8 kwenye kipimo cha rikta, liliharibu zaidi ya nyumba milioni moja na kuharibu barabara ba madaraja makuu. Kazi za kukarabati maeneo yaliyoharibika itakua changa moto kuu ya rais mteule sebastian Pinera anaetarajiwa kuapishwa na kuchukua madaraka katika muda wa wiki mbili zijazo.
Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na mabomba ya maji kutawanya idadi kubwa ya atu walokua wananyakua vitu kutoka maduka katika mji wa pili kwa ukubwa wa Chile wa Concepcion. Wakazi hao walisema tetemeko limewasababisha kupoteza kila kitu na hawakua na njia nyingine ila kunyakua chakula walopata madukani.