Wiki iliyopita Mahakama ya Rufaa nchini Tanzania ilikataa rufaa ya mwanamuziki mashuhuri nchini humo, Nguza Viking - maarufu kama Babu Seya – na mwanawe mmoja Papii Kocha ambaye pia ni mwanamuziki wa kizazi kipya na kuwarejesha gerezani kutumikia kifungo cha maisha.
Lakini mahakama hiyo iliwaachia huru watoto wengine wawili wa Babu Seya - Francis Mbangu na Nguza Mashine – baada ya kuonekana kuwa hawana makosa yoyote baada ya kukaa gerezani kwa miaka sita. Awali Babu Seya na watoto wake hao watatu wa kiume walihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mbali mbali ya ubakaji.
Sauti ya Amerika imezungumza na watoto hao wawili walioachiliwa huru Nguza na Francis-kuhusu hisia zao baada ya kutoka gerezani, maisha yao walipokuwa ndani, walivyopokelewa
baada ya kuachiwa huru, na matumaini ya baba yao na kaka yao hatimaye kutoka jela.