Mvutano uliojitokeza kuhusu madaraka ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kufuatia hatua ya Odinga kuwasimamisha kazi mawaziri wawili unaelekea kupindukia kuwa mgogoro kamili ya kikatiba huku pande za vyama vya PNU na ODM vikiwa vinavutia upande wao.
Mwanasheria Mkuu wa serikali Amos Wako alitamka Jumatatu kuwa Waziri Mkuu hakuwa na madaraka ya kikatiba kuwasimamisha kazi mawaziri wa serikali bila kushauriana na Rais. Lakini muda mfupi kabla ya hapo Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi akielezea msimamo wa chama cha ODM alisema kuwa Waziri Mkuu Odinga alikuwa ndani ya uwezo wa madaraka yake alipochukua hatua ya kuwasimamisha kazi mawaziri William Ruto wa kilimo na Prof. Sam Ongeri wa elimu - hatua ambayo ilitenguliwa saa chache baadaye na Rais Mwai Kibaki Jumapili.
Wakati huo huo, ODM imetoa wito wa kumtaka msuluhishi wa mgogoro wa Kenya mwaka 2007, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan arejee nchini kusuluhisha mgogoro huu wa sasa.
Watalaam wa maswala ya sheria na katiba nchini Kenya pia wanatofautiana, wengine wakisema Waziri Mkuu alikuwa na haki ya kuchukua hatua hiyo na wengine wakisema madaraka hayo yako mikononi mwa rais pekee. Wananchi nao pia wana maoni tofauti, kama yalivyokusanywa hapa na Sauti ya Amerika - VOA.