Wamisri wamesherehekea usiku mzima ushindi wa timu yao ya taifa ya kandanda iliyonyakua kwa mara ya tatu mfululizo Kombe la Afrika la Mataifa huko Luanda, Angola, Jumapili usiku. Naibu kocha Shawky Gharib alisema, "tulikuja kushinda kwa sababu hatukufanikiwa kwenda katika kombe la dunia. Mkakati wetu ulikua ni kushinda michuano yote"
Misiri iliweza kupata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya timu kali ya Ghana ambayo iliweza kuwabana kwa sehemu kubwa ya mchezo huo. Lakini katika dakika ya 85 ya mchezo, Mohamed Gedo Nagy, mchezaji wa akiba na aliyeshuka uwanjani kwa mara ya kwanza katika michjuano hiyo ya kombe la Afrika, aliweza kuliona lango na kuipatia nchi yake goli hilo pekee la ushindi.
Ushindi huo wa Misri unaweka rikodi katika historia ya Kombe la Afrika kwa kua nchi ya kwanza kulinyakua kombe mara tatu mfululizo. Na naibu kocha Gharib anasema haukua ushindi rahisi, kwani ilibidi kupambana na timu nne zitakazoliwakilisha bara la Afrika kwenye Kombe la Dunia huko Afrika KUsini baadae mwaka huu.
Katika kugombania nafasi ya tatu Nigeria iliweza kuishinda Algeria bao moja kwa bila, siku ya Jumamosi.