Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 28, 2023 Local time: 22:02

Yar'Adua kurejea nyumbani karibuni


Makamu Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amesema Rais wa Nigeria Umaru Yar’Adua ambaye yupo Saudi Arabia kwa matibabu hivi karibu atarudi nyumbani. Makamu Rais alisema hayo huko Abuja lakini hakueleza lini Rais Umaru Yar’Adua anatarajiwa kurudi nchini humo.

Bwana Yar’Adua aliondoka Nigeria mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, ambapo alisafiri kwenda hospitali moja ya Saudi Arabia kwa matibabu ya moyo. Pia anasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo.

Jumatano baraza la mawaziri la Nigeria na Bunge walitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu suala la bwana Yar’Adua kuendelea kushika madaraka. Baraza la mawaziri lililoteuliwa na Rais, lilieleza kwamba bwana Yar’Adua ana uwezo wa kuendelea kuongoza nchi.

Bunge lilisema bwana Yar’Adua alitakiwa aliarifu bunge juu ya kile walichokiita likizo yake ya matibabu. Katiba inasema ikiwa maelezo kama hayo yametolewa, Makamu Rais lazima ashikilie wadhifa wa Rais kwa muda.

XS
SM
MD
LG