Serikali ya Kenya imewaachia baadhi ya wabunge wa Somalia ambao walikuwa miongoni mwa watu wapatao 400 waliokamatwa katika msako mkubwa uliofanywa Jumapili mjini Nairobi. Waziri mdogo wa Wizara ya Mifugo, Kenya, Aden Barre Duale, aliambia Idhaa ya Kisomali ya Sauti ya Amerika kuwa wabunge tisa na watu wengine kadha waliachiwa huru Jumatatu mchana baada ya kutokea katika mahakama moja ya Nairobi. Duale alisema wabunge wengine wawili wa Somalia wangali wanashikiliwa kwa sababu za kiuhamiaji.
Mapema, afisa wa ubalozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Aden Edsan, aliambia Sauti ya Amerika kuwa wengi wa watu waliotiwa nguvuni walikuwa na visa na hati halali za kuwepo nchini Kenya. Polisi wa Kenya waliwatia nguvuni wasomali wapatao 400 Jumapili katika eneo la Eastleigh, eneo linalokaliwa na wahamiaji wengi wa kisomali katika mji wa Nairobi.
Kenya inashutumu kundi la kigaidi la Al-Shabab la Somalia kwa kuchochea maandamano na fujo zilizotokea Ijumaa mjini Nairobi na kusababisha vifo vya watu watano. Waandamanaji walikuwa wakipinga kushikiliwa kwa Sheikh wa Kijamaica Abdullah Al-Faisal ambaye Kenya inajaribu kumwondoa nchini humo kwa madai ya kuwa aliingia Kenya kinyume cha sheria.
Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika leo pia ilizungumza na wakili Haron Ndubi wa Nairobi ambaye anawakilisha baadhi ya Wasomali waliokamatwa.