Serikali ya Kenya imesema itasimama kidete pamoja na mataifa mengine 20 ya Afrika kupinga pendekezo la Tanzania kuruhusiwa kuuza pembe zake za ndovu, wakati wa mkutano ujao wa CITES, huko Qarat mwezi Marchi mwaka huu.
Meneja wa uhusiano wa nyama pori nchini Kenya Paul Udoto amesema kuruhusu biashara hiyo kutawawezesha wawindaji haramu kuongeza mashambulio yao dhidi ya ndovu. Anasema mara ya mwisho CITES iliporuhusu baadhi ya mataifa ya Kusini mwa Afrika kuuza sehemu ya sehena yao halali, ndovu 47 waliuliwa na wawindaji haramu na mwaka 2009 ni ndovu 214, hiyo ikiwa idadi ya juu kabisa tangu mwishoni mwa miaka 1980.
Kutokana na hali hiyo Bw Udoto anasema Kenya itashirikiana na mataifa mengine 20 na kuelekea Brussels mwezi ujao ili kuifahamisha Umoja wa Ulaya juu ya hatari za kuruhusu biashara ya ndovu. Tanzania inasema inataka kuuza akiba yake ili kuweza kuimarisha mbuga zake na hasa biasahara ya utali.
Mataifa yanayodaiwa kuchochea biashara hiyo ni yale ya Asia na hasa China ambazo zinahitaji sana pembe hizo zinazojulikana kama "dhahabu nyeupe" kwa ajili ya madawa na mambo mengine mbali mbali.