Wanasiasa wa Nigeria, wasomi, na wanaharakati wa haki za binadamu, wanapanga kufanya maandamano makubwa leo Jumanne, kupinga kutokuwepo kwa Rais nchini humo kwa wiki saba.
Maandamano yanatarajiwa kufanyika katika mji mkuu, Abuja, ambapo bunge pia linatarajiwa kuzungumzia hali ya kisiasa iliyopo tangu Rais kuuguwa. Rais Umaru Yar’Adua hajaonekana au kuzungumza hadharani tangu mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, ambapo alipelekwa hospitali moja huko Jedda, Saudi Arabia.
Wakosoaji wanasema kuendelea kutokuwepo kwa Rais huyo kunakiuka katiba na ameiacha nchi katika hatari. Mahakama moja ya serikali, itasikiliza kesi tatu Jumanne, zinazotaka Rais huyo amwachie madaraka makamu Rais wake Goodluck Jonathan.
Siku ya Jumatatu, msemaji wa Rais alikanusha uvumi kwamba bwana Yar’Adua amekufa au yupo kwenye koma. Msemaji huyo Olusegun Adeniyi, aliwaambia waandishi wa habari kwamba bwana Yar’Adua yupo hai na kwamba anapata nafuu. Alisema Rais yupo makini na anazungumza na maafisa wa Nigeria kwa njia ya simu.