Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa umeme kwa zidi ya wiki moja sasa na kusababisha upungufu mkubwa wa maji, na bei ya maji inayopatikana kupanda kwa zaidi ya marudufu. Jambo lililowakasirisha sana wakazi wa Unguja na Pemba hasa kusikia kwamba huwenda wasiwe na umeme kwa mwezi mmoja.
Waziri wa nchi katika afisi ya waziri mkuu, Bw. Hamza Hassan Juma amesema kwamba, chombo kingine muhimu kimeripuka katika mtambo wa umeme baada ya kupokea chombo kilichoharibiki wiki iliyopita kutoka Afrika Kusini.
Bw Hassan Juma anasema tatizo litachukua muda huo wote kwa sababu huu ni wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka na hivyo ni vigumu kupata huduma za kuchonga chombo kingine huko Afrika Kusini.
Zainab Ali Mkazi wa Zanzibar akieleza tafrani zake ambazo zinaelezwa na Wazanzibari wengi ni kwamba hivi sasa wanalazimika kununua maji kwa bei ya juu kabisa, chakula kimeanza kpunguka, na hali ni mbaya wakati huu wa joto.
Wafanyabiashara nao wameingia na wasi wasi mkubwa hasa wakati huu wa msimu wa watali. Simai Mohamed Juma mwenyekiti wa wafanyabishara Zanzibar anasema ingawa hoteli kuu na biashara muhim wana mitambo yao ya umeme lakini tatizo kuu ni kupata chakula na samaki wakutosha.