Tanzania ilikumbwa na msiba Ijumaa ambapo watu 19 walipoteza maisha yao katika ajali ya barabarani. Akizungumza katika kipindi cha Meza ya Waandishi wa Habari, Mhariri Rashid Kejo wa gazeti la Mwananchi, alisema basi la Mohammed Trans lililokuwa likitokea Nairobi, Kenya, liligongana na basi dogo lililokuwa limebeba abiria 19 kutoka Dar Es Salaam, wakielekea Moshi kwenye harusi.
Kejo anasema abiria wote 19 waliripotiwa kufa katika ajali hiyo iliyotokea wilaya ya Same katika mkoa wa Kilimanjaro na kwamba marehemu walitoka katika familia tatu.
Akishiriki katika kipindi hicho cha meza ya waandishi wa habari, mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Rwanda, Silvanus Karemera, alieleza kuwa mahakama ya kimataifa ya Arusha-ICTR, ambayo inasikiliza kesi za watuhumiwa wa mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda mwaka 1994, imeongezewa muda wa kuhudumu shughuli zake hadi mwaka 2012.
Karemera alisema serikali ya Rwanda imechukizwa na hatua hiyo, ikisema kuwa mahakama hiyo ya Arusha inatumia dola bilioni moja za kimarekani kila mwaka, lakini tangu ilipoanzishwa miaka 10 iliyopita, utekelezaji wake wa kazi hauridhishi.
Serikali ya Rwanda inasema mahakama ya ICTR, imesikiliza chini ya kesi 40 tangu kutokea kwa mauaji hayo nchini humo.