Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 20, 2024 Local time: 22:56

Suala la Ardhi EAC Lafafanuliwa


Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuia ya Afrika mashariki Dk. Deodoras Kamara wa Tanzania, ametoa ufafanuzi jinsi suala la ardhi litakavyoshughulikiwa katika nchi wanachama wa jumuia hiyo, wakati huu ambapo nchi hizo zimetia saini mkataba wa soko la pamoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, siku ya Jumanne mwenyekiti wa Jumuia hiyo ambaye pia ni Waziri wa Wizara ya Afrika Mashariki Tanzania, Dk Kamara, amesema suala la ardhi ndani ya jumuia hiyo litashughulikiwa kwa kadri nchi husika linavyolitazama kwa mujibu wa katiba na sheria zake.

Dk. Kamara alizungumzia pia suala la Congo na Sudan kusini kutaka kujiunga ndani ya jumuia hiyo. Alisema “na kama tukishatengeneza ukanda huru wa kibiashara wa SADC, COMESA na EAC, ni wazi kwamba nchi ya Congo na Sudan watakuwa wameingia kwenye jumuia hiyo. nchi hizo kuingia kwenye jumuia si suala baya kwa misingi ya uchumi”.

Ameelezea kuwa ili kujiunga na jumuia hiyo kuna vigezo kabla ya kupitishwa kuwa mwanachama ambapo ni pamoja na kuulizwa iwapo serikali ya nchi yako ina utawala bora, pili, sera za nchi yako ziwe zinafuata uchumi wa soko na tatu utumiaji wa lugha ya Kiswahili na Kingereza. Masuala haya matatu hayana mjadala ni lazima uyafuate na kukubaliana nayo.

Kwa upande mwingine maonesho ya wajasiriamali, maarufu kama juakali, wanachama wa jumuia ya Afrika Mashariki yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar Es salaam. Akizungumzia maonesho hayo, naibu Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana nchini Tanzania, Dk.Makongoro Mahanga, amezishauri serikali za jumuia ya Afrika Mashariki kuwasaidia wajasiriamali ndani ya jumuia hiyo kwa kuwajengea mazingira ya kupata mitaji, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi hizo zimetia saini mkataba wa soko la pamoja.

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG