Rais Barack Obama wa Marekani na mwenyeji wake wa China Hu Jintao walikutana kwa kikao cha pili cha mazungumzo yao mjini Bejing, kujadili masuala magumu ya uchumi na masuali mengine.
Baada ya mazungumzo yao, viongozi hao walikutana na wandishi habari bila ya kupokea masuali kutoka kwa wandishi. Walisema mazunguimzo yao yalizingatia juu ya namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, na kukabiliana na changa moto zinazokabili dunia wakati huu.
Rais Obama alisema walizungumza pia namna ya kuihimiza Korea ya Kaskazini kurudi kwenye mazungumzo ya mataifa sita juu ya mpango wake wa nuklia.
Rais Hu alimkaribisha rasmi Bw Obama katika sherehe iliyofanyika katika ukumbi wa wananchi, "Great Hall of the People" siku ya Jumanne.
Bw Obama alikua na duru ya kwanza ya mazungumzo na Bw Hu siku ya Jumatatu.
Siku hiyo hiyo aliwambia wanafunzi mjini Shanghai kwamba anaunga mkono kutumia kwa uhuru mtandao, jambo ambalo China inaweka vizuwizi vikali. Alizungumzia juu ya kile alichoikieleza haki za kimataifa za kujieleza kisiasa, uhuru wa kuabudu na uhuru wa habari.
Bw Obama alizungumzia masuala hayo yote wakati wa mkutano ulofanyika ndani ya ukumbi wa chuo kikuu cha Shanghai katika kikao cha masuali na majibu na wanafunzi. Alisema lazima kila nchi iheshimu nchi nyingine na haijalazimu taifa moja kulazimisha mfumo wa serekali yake kwa taifa jingine.
Mkutano huo na wanafunzi ulitangazwa moja kwa moja kwenye ukurasa wa tovuti ya White house lakini serekali ya China ilidhibiti kwa makini jinsi vyombo vya habari vilifuatilia mkutano huo ndani ya nchi hiyo.