Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 03:43

MDC yatoa siku 30 za suluhisho Zimbabwe


Waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai, anasema chama chake kimemaliza sehemu ya mgogoro na serikali ya kushirikiana madaraka na kimempa Rais Robert Mugabe mwezi mmoja kutatua tofauti zilizopo katika ushirika huo.Bwana Tsvangirai alitoa tamko hilo mwisho wa mkutano wa kisiasa na timu ya ulinzi ya jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC.

Wanachama wa kundi hilo, wakuu wa nchi za Zimbabwe, Zambia na Swaziland walimaliza mkutano huko Msumbiji kwa kuvisihi vyama katika serikali ya umoja wa Zimbabwe kutatua tofauti zao, chini ya mpatanishi wa mgogoro huo Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma. Bwana Tsvangirai alisema anakubali uamuzi wa SADC.Bwana Mugabe pia alihudhuria mkutano huo lakini hakutoa matamshi yeyote.

Bwana Tsvangirai alitangaza wiki tatu zilizopita kwamba chama chake cha Movement for Democratic Change-MDC, kitasusia mikutano ya baraza la mawaziri na kujihusisha na shughuli za mawaziri wa chama cha Rais Robert Mugabe cha ZANU-PF.

Alikishutumu chama cha ZANU-PF kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu mkataba wa kushirikiana madaraka uliotiwa saini zaidi ya mwaka mmoja uliopita.Pia alikishutumu chama cha ZANU-PF kwa kujaribu kuyumbisha serikali ya umoja na kuanzisha tena kampeni za kuwakamata na kuwadhalilisha wafuasi wake wa chama cha MDC.

Bwana Mugabe alikishutumu chama cha MDC kwa kushindwa kumaliza vikwazo vya kiuchumi, ambavyo alisema vinaumiza uchumi wa Zimbabwe.

Viongozi wa SADC walitoa taarifa kufuatia mkutano unaowasihi viongozi wa Zimbabwe kushiriki kwenye mazungumzo kwa ajili ya kuimarisha hadhi na makubaliano ya mkataba wa kushirikiana madaraka.Taarifa hiyo pia ilisihi viongozi hao kuzuia kuendeleza mgogoro wa hali iliyopo sasa.

XS
SM
MD
LG