Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 25, 2025 Local time: 12:08

Ocampo ataomba uchunguzi kuhusu ghasia Kenya


Wananchi wa Kenya wamepokea kwa hisia tofauti matamshi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu-ICC, Luis Moreno Ocampo, kwamba ataiomba mahakama hiyo kuanzisha uchunguzi dhidi wahusika katika ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari pamoja na viongozi wa Kenya, Ocampo alisema atapeleka ombi lake la kufanyika uchunguzi kwa ICC mwezi Disemba. Pia amesema ataifanya Kenya kuwa mfano wa dunia katika masuala ya ghasia za kisiasa. Amesema atawachukulia hatua wale wote waliohusika kwa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu na mapigano ya kikabila ambayo yaliuwa watu 1,300 mwanzoni mwa mwaka 2008.

Matamshi ya Ocampo yameibua hisia tofauti nchini humo, huku baadhi ya wananchi wakisema mahakama ya ICC sasa ina nafasi nzuri kuhakikisha wahusika wakuu waliochochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu uliopita wanafikishwa mahakamani.

Lakini suala linalowachanganya watu wengi ni kuhusu jinsi watuhumiwa waliopanga na kuchochea ghasia watakavyopelekwa kwenye vyombo vya sheria kwani baadhi yao ni mawaziri wenye ushawishi mkubwa katika serikali ya muungano.

XS
SM
MD
LG