Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:52

Rais Mugabe na Tsvangirai washindwa kuelewana


Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na waziri mkuu Morgan Tsvangirai wameshindwa kutatua tofauti zao, katika mkutano wao wa kwanza tangu chama cha bwana Tsvangirai kilipojitoa kwenye serikali ya umoja wa kitaifa, siku 10 zilizopita.

Msemaji wa chama cha waziri mkuu cha MDC, anasema viongozi hao wawili wametofautiana juu ya masuala muhimu yanayoathiri serikali ya umoja wa kitaifa, hata ingawa walikutana kwa saa tatu jana Jumatatu mjini Harare. Msemaji huyo Nelson Chamisa, alisema MDC itasubiri matokeo ya juhudi za mazungumzo ya jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC.

Bwana Chamisa alisema ikiwa mazungumzo hayo yatashindikana, chama cha MDC kitaanza kujiandaa kwa uchaguzi mpya. Hakukuwa na matamshi ya haraka kuhusu hali ya mazungumzo ya kisiasa kutoka kwa bwana Mugabe au chama chake cha ZANU-PF. Bwana Tsvangirai alisema Octoba 16 kuwa chama cha MDC hakitafanya kazi tena na chama cha ZANU-PF, ambapo anasema chama hicho kimekuwa cha kilaghai na rafiki asiyetabirika. Hatua hii inafuatia kukamatwa kwa mmoja wa wafanyakazi wa bwana Tsvangirai, mkulima mweupe Roy Bennett kwa shutuma za ugaidi.

Ijumaa iliyopita polisi wa Zimbabwe, walipekuwa nyumba inayomilikiwa na chama cha bwana Tsvangirai cha MDC, na kuongeza mivutano zaidi. Chama cha MDC kinasema mawaziri kutoka jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC, wanaohusika na masuala ya siasa, ulinzi na usalama watazungumzia suala hilo siku ya Alhamisi mjini Harare.

XS
SM
MD
LG