Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 09, 2024 Local time: 19:31

Hakuna anayestahili tuzo la Mo Ibrahim 2009


Wakfu unaotoa tuzo la dola milioni 5 kwa utawala bora barani Afrika, unasema haujampata kiongozi yeyote wa kumtunuku zawadi hiyo mwaka huu. Katika taarifa yake ya jana Jumatatu, Wakfu wa Mo Ibrahim ulisema kamati yake ya tuzo iliwafikiria baadhi ya wagombea, lakini kufikia mwisho haikuweza kumchagua mshindi.

Mfanyabiashara tajiri wa Sudan, Mo Ibrahim, ambaye anaongoza taasisi hiyo anasema uamuzi huo usionekane kwamba ni dalili za kutothamini mchango wa viongozi, na anaongeza kuwa wakati mwingine hakuna mshindi anayepatikana. Tuzo hilo hutolewa kwa kiongozi wa zamani wa Afrika aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, ambaye hakiuki masharti ya muhula wake na kuondoka madarakani ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Wajumbe wa kamati hiyo walisema hawakuweza kuzungumzia hatua za uamuzi wao. Washindi wa awali wa tuzo hizo ni marais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Alberto Chissano na Festus Mogae wa Bostwana. Viongozi wote hao wawili waliachia madaraka baada ya kumaliza mihula miwili. Kamati hiyo ya tuzo inaongozwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan na inawahusisha viongozi sita maarufu wa kisiasa, akiwemo Mohamed ElBaradei, mkurugenzi wa taasisi ya nishati ya kimataifa ya Atomic.

Tajiri huyo mzaliwa wa Sudan Mo Ibrahim alianzisha taasisi hiyo mwaka 2007, kuimarisha utawala bora barani Afrika, ambapo viongozi wengi wanajiongeza muda madarakani na kuruhusu rushwa kutawala serikali zao. Taasisi hiyo inasema mkutano wake wa mwezi Novemba utafanyika Dar- es Salaam nchini Tanzania kama ulivyopangwa japokuwa hakuna mshindi.

XS
SM
MD
LG