Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 28, 2022 Local time: 18:38

Ghana yachukua kombe la Dunia chini ya miaka 20


Timu ya vijana ya taifa ya Ghana (Black Satellites) wenye umri chini ya miaka 20 kwa mara ya kwanza wameandika historia ya kupeleka kombe la dunia la vijana nchini humo na barani Afrika baada ya kuwabwaga mabingwa wa kombe hilo mara nne Brazil kwa njia ya penalty 4-3.

Mchezo huo wa fainali uliofanyika katika uwanja wa soka wa kimataifa wa Cairo Misri ulishuhudiwa na watu wapatao 67,814 na ulimwengu kwa ujumla ulishuhudia Ghana wakiangusha vigogo wa soka duniani Brazil baada ya mchezo kumalizika ndani ya dakika 90 bila mshindi 0-0.

Mchezo huo ulikwenda dakika za nyongeza pia bila mshindi na Ghana waliopoteza mchezaji wao Daniel Addo mapema katika kipindi cha kwanza kunako dakika ya 37 kwa kadi nyekundu lakini hawakurudi nyuma na kuendeleza mapambano huku wakijibu mashambulizi ya Brazil.

Brazil wakiongozwa na washambuliaji wao hatari Alan Kardec na Desouza walikosa nafasi kadhaa huku wakiwa wametawala mchezo huo katika kiungo na ushambuliaji lakini Ghana kwa upande wao wanastahili sifa kwa kutokukata tamaa na alikuwa ni golikipa wao Daniel Agyei aliyefanya kazi ya ziada kuokoa mashuti kadhaa yaliolekezwa langoni mwake.
Ghana waliingia kwenye fainali hizo baada ya kuitoa Hungary kwa jumla ya mabao 3-2.

Ghana walitolewa kwenye fainali mara ya kwanza 1993 na hao hao Brazil na walikosa nafasi hiyo tena mwaka 2001 baada ya kuangukia pua mbele ya Argentina.
Brazil walichukua kombe hili kwa mara ya mwisho mwaka 2003. Na katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Hungary waliishinda Costa Rica kwa njia ya penati baada ya mpira kumalizika kwa sare ya bao 1-1.


XS
SM
MD
LG