Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:19

Ocampo kukutana na viongozi wa Kenya wiki ijayo


Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC Louis Moreno Ocampo, anatarajiwa kuwasili nchini Kenya wiki ijayo kwa mazungumzo na Rais Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga, kuhusu kufikishwa mahakamani kwa viongozi mashuhuri wa kisiasa waliohusika na ghasia pamoja na mauaji ya baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2007. Pia katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa bwana Kofi Annan anatarajiwa kuwasili nchini humo siku ya Jumapili.

Bwana Louis Moreno Ocampo sasa anatarajiwa kuwasili nchini humo kuzungumzia juu ya utaratibu wa kutekeleza majukumu ya kimahakama baada ya serikali ya Kenya kushindwa kubuni mahakama maalumu kwa ajili wa washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini humo.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa bwana Kofi Annan, ambaye alisaidia kumaliza uhasama wa kisiasa na uongozi kati ya Rais Kibaki na bwana Odinga, na kupelekea kuundwa kwa serikali ya mseto atakuwepo nchini humo kwa ziara ya siku nne.

Lengo kuu la Ziara hiyo ni kukutana na Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga, kabla ya kushauriana na kundi linalohusika na majadiliano na kufikia maridhiano baada ya machafuko ya kisiasa ya muda wa miezi miwili yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 kuuwawa na wengine laki sita kukoseshwa makazi na mali ya thamani kubwa kuteketezwa kwa moto.

Bwana Kofi Annan pia atakutana na viongozi mbali mbali wa kidini, wafanyabiashara, na wanaharakati wa haki za binadamu. Katibu mkuu huyo wa zamani na mwendesha mashtaka mkuu bwana Ocampo, walitoa muda wa kutosha kwa serikali ya mseto ya Kenya hadi tarehe 30 ya mwezi uliopita kwa serikali ya nchi hiyo kuunda mahakama ya kuwashtaki watuhumiwa waliochochea ghasia hizo. Serikali ya mseto ya Kenya haijafanya lolote juu ya kuundwa kwa mahakama hiyo.

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG