Na mwandishi wetu Lisa Schlein
Shirika la Afya Duniani-WHO, limesema wilaya ya Ezo huko Sudan Kusini iko katika hatari kubwa ya kukumbwa na mlipuko wa maradhi. Shirika hilo limesema huduma za afya katika eneo hilo zimeharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kundi la waasi la Uganda la LRA.
WHO imesema waasi wa Lord’s Resistance Army wanaendelea na kampeni yao ya vitisho katika jimbo la Western Equitorial huko Sudan Kusini. Mashambulizi hayo ya LRA yameongezeka katika wiki za karibuni, na yameripotiwa kusababisha zaidi ya watu elfu 80 kukimbia makazi yao.
Umoja Mataifa inaripoti kuwa wilaya ya Ezo ambayo iko karibu na mipaka ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, imekuwa ikishambuliwa kila mara na waasi hao wa Uganda katika miezi ya karibuni.
Kati kati ya mwezi August, kundi la Lord’s Resistance Army lilifanya mashambulizi ya uporaji, kuchoma moto nyumba na makanisa, kuua na kuwajeruhi wananchi na kuwateka nyara wasichana 10. Msemaji wa WHO, Paul Garwood, aliiambia Sauti ya Amerika kwamba waasi hao pia walivamia vituo vya afya.