Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 23:23

Marekani yasikitishwa na uteuzi wa Kibaki


Serikali ya Marekani imesema imesikitishwa na uamuzi wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya kumteua tena mkurugenzi mkuu wa tume ya kupambana na rushwa nchini humo Jaji Aaron Ringera, kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Bunge la Kenya pia limeamua kusimamisha matumizi ya fedha ya tume hiyo ya serikali kama hatua ya kupinga uteuzi huo wa Jaji Ringera. Uamuzi wa Rais Kibaki unaendelea kuzusha hamasa na lawama kali kutoka kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, watu binafsi na ofisi za kibalozi zilizopo nchini Kenya.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya ubalozi wa Marekani mjini Nairobi imesema serikali ya Marekani inasikitishwa na uamuzi na utaratibu uliotumiwa kumteua Jaji Ringera kuwa mkurugenzi wa tume hiyo ya serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano, bila kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa hasa kutokana na kazi mbaya iliyotekelezwa na Jaji Ringera kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

Katika taarifa yake, ubalozi wa Marekani nchini Kenya unasisitiza kwamba uteuzi huo unastahili kufanywa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na kwa njia ya mashauriano. Marekani inasema ipo tayari kuunga mkono madai ya wananchi kuhusu utekelezaji wa mabadiliko muhimu kwenye serikali kuambatana na makubaliano yaliyoafikiwa wakati wa mazungumzo ya katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan.

Wananchi pia wamekasirishwa na uteuzi huo kutokana na kazi duni iliyofanywa na tume hiyo kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG