Wataalamu wa masuala ya katiba pamoja na wawakilishi wa vyamavya kisiasa 47 nchini Kenya, wanahudhuria kongamano la siku mbili linalojadili marekebisho ya katiba nchini humo.
Hii ni mara ya kwanza kwa wataalamu wa masuala ya katiba na wawakilishi wa vyama vya kisiasa kushauriana kuhusu marekebisho ya katiba baada ya kuundwa kwa serikali ya mseto nchini humo.Kila chama kinawakilishwa na wajumbewawili kwenye kongamano hilo.
Kulingana na tume iliyoundwa na bunge kushughulikia masuala ya katiba, zoezi hili linatarajiwa kumalizika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2012, ili kutoa nafasi kwa wananchi na bunge la taifa nchini humo kutoa maoni yao.
Baadhi ya masuala nyeti yanayoshughulikiwa na wajumbe wanaohudhuria kongamano hilo yanahusu mfumo wa serikali ijayo nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na majukumu yanayostahili kutekelezwa na ofisi ya rais iwapo Kenya itazingatia mfumo wa serikali ya waziri mkuu mwenye cheo na uwezo wa kuunda baraza la mawaziri.