Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 24, 2024 Local time: 11:43

Wafungwa 18 Wafa Jela Nchini Kenya.


Wafungwa 18 wamefariki katika gereza la Kodiaga wilayani Nyanza nchini Kenya baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu na homa ya mapafu. Taarifa juu ya vifo vyao imezua shutuma kali kutoka kwa tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu.

Makamu rais wa tume hiyo Bwana Hassan Omar, aliiambia Sauti ya Amerika kuwa wakuu wa gereza hilo wanawajibu kuhakikisha wafungwa wanapewa huduma za matibabu kama mojawapo ya haki zao za kimsingi. Omar alisema tume hiyo ya kutetea haki za binadamu ilishangaa ni kwa nini maafisa wa gereza hilo hawakumtenga na kumpeleka hospitali mfungwa wa kwanza aliyegunduliwa kuwa na maradhi ya kifua kikuu.

Kifua kikuu huambukiza kwa kasi na huwenda watu wengine katika gereza hilo wakiwemo walinzi wakajikuta wameambukizwa. Bwana Omar alisema hali kwa jumla katika magereza ya Kenya ni ya kusikitisha. Walinzi wanafanya kazi katika mazingira magumu na ingawa serikali inajitahidi kuimarisha hali hiyo, bado kuna mengi ya kufanya kufikia kiwango kinachotakiwa. Tume hiyo imeahidi kufuatilia kesi juu ya vifo vya wafungwa hao na kuwashitaki wale watakaokutwa na hatia ya kuzembea katika wajibu wao.

XS
SM
MD
LG