Tume ya uchaguzi Zanzibar, ZEC, imetangaza kwamba haitaendelea na zoezi la kuaandikisha wapiga kura kwenye daftari la kudumu huko Pemba hadi itakapo kamilisha uchunguzi utakaohakikisha kuwa kasoro zilizojitokeza hazitorudia tena.
Mwenyekiti wa ZEC Khatibu Mwinchande, amesema ili zoezi hilo liweze kuendelea, ni vyema wanasiasa wakasafisha kile alichokieleza "njia ambayo itawasaidia wananchi wengi kujitokeza kwa ajili ya kuandikishwa katika daftari hilo."
Mwinchande alitoa kauli hiyo baada ya zoezi hilo kusimamishwa kwa muda usiojulikana kufuatia wananchi wa jimbo la Ole kugomea zoezi hilo, wakipinga hatua ya kutoandikishwa wapiga kura wasiokua na vitambulisho vya ukaazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Kadi za Vitambulisho Zanzibar, Bw Mohamed Juma Ame, ambae alisema ni makosa kwa Masheha kuwanyima wananchi fomu za maombi ya vitambulisho vya ukaazi, jambo ambalo limepelekea kusitishwa kwa zoezi la uandikishaji kwa muda usojulikana.
Bw Juma Ame anasema, "Sheha ambaye kwa matakwa yake anamnyima mtu fomu, Sheha wa namna hiyo anavunja sheria. Na atakaporipotiwa kwetu, basi tutafuata utaratibu na kutekeleza. kwa sababu sheria nambari 7 ya mwaka 2005, inaeleza wazi, kwamba mtu yeyote atakae mnyima haki mtu ambae anastahiki anatakiwa ashtakiwe kisheria."
Kiongozi wa upinzani bungeni Hamad Rashid wa chama cha CUF anasema "kuingiza kifungu kinachomtaka Mtanzania Mzanzibari ni kinyume cha katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kifungu cha saba na vile vile kinyume na katiba ya Zanzibar kifungu cha tano." Sheria hiyo anasema wanaoina ni batili na imeleta mgogoro mkubwa sana. Kwa hivyo anasema "ni dhahiri uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakua na kasoro ya kisheria kwa maana ya kuvunjwa katiba kwa kutumiwa daftari la wapiga kura la Zanzibar, ambalo lenyewe wapiga kura wake wamepatikana kinyume cha katiba ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."