Usafirishaji na biashara haramu ya kuuza binadamu inazidi kushika kasi katika bara la Afrika, ambapo nchini Tanzania zaidi ya wageni 2,163 wamekamatwa wakiwa mbioni kusafirishwa kwenda nchi mbali mbali.
Idadi hiyo ya watu waliokuwa wakisafirishwa isivyo halali ni takwimu ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, kuanzia mwezi Januari mwaka 2008 hadi mwezi Juni mwaka huu.
Taarifa inasema watu 1,600 walikamatwa katika kipindi cha mwaka jana na wengine 563 wamekamatwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Juni mwaka huu.
Raia hao waliokuwa wakisafirishwa katika biashara hiyo haramu ya usafirishaji watu, wengi ni wa Ethiopia na wa Somali, ambapo wamekamatwa hapa nchini Tanzania wakiwa njiani kwenda nchi za kusini mwa Afrika na ulaya tayari kwa kuuzwa.