Serikali ya kenya imethibitisha kupokea taarifa za ugonjwa huo na kusema tayari wataalamu wamepelekwa katika maeneo hayo kwa lengo la kujua ni ugonjwa gani na namna ya kuwasaidia wananchi hao.
Waziri wa Afya Beth Mugo alisema Jumanne kuwa vipimo vilivyochukuliwa vinaonyesha kuwa baadhi ya watu waliokuwa wakilalamika walikuwa wanaumwa kipindupindu na wengine walikuwa wanaharisha damu.
Waziri Mugo alisema kuwa uchunguzi unaendelea katika maabara za nchi hiyo na kwamba mara tu baada ya kupata matokeo ya uchunguzi huo, serikali itawatangazia wananchi.
Lakini kwa sasa Bi. Mugo ametoa ushauri kwa wananchi kuzingatia hali ya usafi ili kujiepusha na uwezekano wa kuugua kipindupindu. Miongoni mwa hatua alizotaja ni kusafisha mikono mara kwa mara, na hasa kabla na baada ya kula chakula, na kuosha matunda kabla ya kula.