Maafisa na wanadiplomasia katika kisiwa hicho kilichopo bahari ya Hindi wanasema Rais Marc Ravalomanana wa Madagascar alisaini waraka Jumanne wa kukabidhi madaraka kwa bodi ya maofisa wa juu wa jeshi la nchi hiyo.
Profesa Charles Bwenge wa chuo kikuu cha Florida nchini Marekani, anasema kuna haja kwa viongozi wa Afrika kutathimini kwa kina chanzo cha mgogoro wa Madagascar kabla ya kuamua hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Aidha Profesa Bwenge alisema kuwa kama ilivyokuwa kwa Kenya, Zimbabwe na mataifa mengine kadhaa ya Afrika, mapinduzi nchini Madagascar yamefanyika kwa kutumia mtindo mpya ambapo viongozi waliopo madarakani wanashinikizwa na upinzani kujiuzulu au kushirikiana madaraka.
Nchini Madagascar upinzani ambao unaongozwa na Andry Rajoelina umeshirikiana na jeshi kumshinikiza Rais Ravalomanana ajiuzulu.