Na: Timothy Kaberia
Rais Obama hapati mteremko katika kupitishwa bajeti huku wademokrat na warepublikan wakiendelea kubishana kuhusu mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2010. Wademokrat wengi na maafisa wa utawala wa Obama wanasema muda zaidi unahitajika ikiwa hatua zilizochukuliwa za kufufua uchumi wa Marekani zitazalisha matunda. Maafisa wa White House wanasema hawatilii maanani fununu kuhusu uwezekano wa mpango wa pili wa kufufua uchumi zaidi ya ule wa dola bilioni 787 zilizoidhinishwa mwezi uliopita.
Viongozi wa wademokrat ikiwa ni pamoja na spika wa bunge Nancy Pelosi wanasema kwa sasa lengo lao ni kuhakikisha kwamba mabilioni ya dola zilizoidhinishwa na bunge na kutiwa saini na rais Obama zimetumika kwa njia ya kuwajibika. Bi Pelosi alikanusha madai kuwa wademokrat wameanza kuandaa mpango wa pili wa kuchochea uchumi.
Lakini maseneta na wawakilishi wa chama cha republikan alhamisi waliendelea kukosoa mapendekezo ya bajeti ya rais Obama kwa mwaka 2010. Seneta John Sessions na mwakilishi Paul Ryan walisema bajeti hii kimsingi ni ongezeko la kodi, matumizi zaidi na deni zaidi.Baadhi ya wademokrat pia wameeleza wasiwasi wao kuhusu vipengele fulani vya bajeti hiyo. Kwenye mkutano na maafisa wa majimbo rais Obama na makamu wa rais Joe Biden walirejea azma yao ya kuhakikisha kwamba fedha za serikali zinatumika kwa kuwajibika na kuongeza kuwa matumizi mabaya yakigunduliwa serikali itachukua hatua ipasavyo. Bunge linapitia mapendekezo ya bajeti.