Rais mteule wa Marekani Barack Obama ataapishwa Januari 20 kuwa rais wa 44 wa taifa hilo imara duniani, huku kukiwa na matumaini makubwa kuwa ataweza kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili watu wengi duniani.
Franklin Wambugu, mtangazaji wa televisheni na radio ya Citizen nchini Kenya, amesema Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo wananchi wameweka imani na matumaini makubwa kwa uongozi ujao wa 'Rais Obama.'
Wambugu amesema pia kuwa mbali na matarajio hayo, ushindi na hatimaye urais wa Barack Obama ambaye ni mtoto wa baba mkenya, ni historia kubwa kuwahi kutokea Marekani.
Naye BMJ Mureithi, mwandishi habari kutoka Atlanta Georgia, amesema rais mteule Obama atasafiri kwa gari moshi akitokea Philadelphia kuelekea Washington, DC ambapo sherehe za kuapishwa kwake zitafanyika. Hali ya usalama imeimarishwa kwa kiwango cha juu mno kuwahi kuonekana katika sherehe zozote Marekani.