Umoja wa Afrika umesema hautatumia nguvu kumwondoa madarakani rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, na wachambuzi wa siasa wanasema hawaamini Umoja wa Mataifa utafanya chochote kwasababu matatizo ya Afrika hayajawahi kupewa kipaumbele.
Akiongea na Sauti ya Amerika, mhariri wa gazeti la Daily Nation la Kenya Mutuuma Mathiu, amesema haamini kama serikali ya Kenya au waziri mkuu Raila Odinga ataendelea kudai matumizi ya nguvu dhidi ya rais Mugabe.
Bwana Mathiu amesema haamini mataifa ya Afrika au Umoja wa Mataifa utachukua hatua ya kumuondoa madarakani rais Mugabe ambaye anasema hana haki yoyote ya kuiongoza Zimbabwe.
Hatahivyo, amewalaumu wananchi wa Zimbabwe kwa kushindwa kuchukua msimamo mkali dhidi ya serikali ya Mugabe, lakini akaomba jumuiya ya kimataifa kuendelea kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu wa Zimbabwe.