Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 22:43

Mapigano Yaendelea DRC


Mapigano kati ya wana mgambo wa Mai mai na waasi wa CNDP wanao ongozwa na Jenerali Laurent Nkunda, yameingia siku ya pili huku kukiwa na wasiwasi kuhusu mauwaji ya raia wanao jaribu kukimbia mapigano hayo.

Msemaji wa waasi wa CNDP Bertrant Bisimwa ameiambia Sauti ya Amerika kuwa hana uhakika kama kuna raia ambao wameuwawa, lakini pia akasema kuwa palipo na mapigano, kuna uwezekano mkubwa kwa raia kupoteza maisha.

Bwana Bisimwa amesema, "Inawezekana kuna kuwa na raia ambao wameuwawa, inawezekana," na kuongeza kuwa inasikitisha kuona raia wanakufa katika mapigano nchini Congo.

Gavana wa jimbo la Kivu ya Kaskazini, Julien Paluku amesema kuwa waasi wa Nkunda wanaendesha mauwaji ya kiholela kwa vijana wanao washuku kuunga mkono wana mgambo wa Mai mai.

Gavana Paluku amesema maeneo hayo ambapo mauwaji hayo yanadhaniwa kufanyika yako mikononi mwa waasi, na kuomba walinzi wa amani wa umoja wa mataifa kuhakikisha raia hawaendelei kuuwawa na waasi hao.

Hata hivyo amesema idadi kamili ya vijana ambao wameuwawa haijajulikana, lakini anategemea kupata ripoti kamili kutoka kwa maofisa wa mpango wa kulinda amani wa umoja wa mataifa MONUC ambao wamekwenda eneo la mapigano kufanya tathimini ya mauwaji hayo na hali ya kibinadamu kwa ujumla.

Aidha Gavana Paluku ameishutumu kwa mara nyingine tena serikali ya Rwanda kuwa inawasaidia waasi wa Nkunda na kwamba kuna ushahidi wa kuthibitisha hilo.

Nkunda na wapiganaji wake wamekuwa wakipigana na majeshi ya serikali ya rais Joseph Kabila kwa madai kuwa anajaribu kulinda maslahi ya watusi wanaoishi nchini humo.

Wakati huo huo, umoja wa mataifa unasema waasi wamekamata mji mwingine wa Nyanzale kutoka majeshi ya serikali.

XS
SM
MD
LG