Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 18, 2024 Local time: 23:38

Ruto, Ongeri Wasimamishwa Kazi


Kenya imewasimamisha kazi kwa muda wa miezi mitatu mawaziri wa Elimu Professa Sam Ongeri na William Ruto wa Kilimo wakati uchunguzi unaendelea kuhusu kashfa za rushwa kubwa katika wizara zao.

Waziri Mkuu Raila Odinga alitangaza hatua hiyo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi Jumapili mchana, akisema kwamba hatua hiyo imefuata mashauriano ya kina ndani ya serikali.

Jumamosi serikali ilitangaza kuwasimamisha kazi maafisa waandamizi wanane ikiwa ni pamoja na makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa mashirika ya umma yaliyotajwa katika kashfa za rushwa kuhusu fedha za misaada ya elimu na ruzuku ya mahindi. Waliokumbwa na hatua ya Jumamosi ni pamoja na makatibu wakuu Dr. Romano Kiome (Kilimo), Ali Mohammed (Mipango Maalum), Prof. Karega Mutahi (Elimu) na Dr. Mohammed Isahakia (Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Odinga alisema Jumapili hatua ya kuwasimamisha pia mawaziri Ruto na Ongeri imefuatia ripoti za taasisi za kukagua mahesabu ambazo zimeonyesha ubadhirifu wa fedha ulitokea katika wizara hizo mbili.

Ripoti iliyotolewa wiki iliyopita kuhusu kashfa ya mahindi ilisema kuwa karibu Sh. billioni 2 zilipotea katika uuzaji wa mahindi ya ruzuku. Wizara ya Elimu inakabiliwa na shutuma ya wizi wa karibu Sh millioni 103 za misaada ya kutoa elimu ya msingi bure. Misaada hiyo ilitoka Uingereza na Marekani ambazo sasa zimesimamisha misaada hiyo.

XS
SM
MD
LG