Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 08, 2024 Local time: 21:30

Mvua kubwa zinazoendelea China zauwa watu sita


Picha ya majengo yalioharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha China.Picha ya maktaba Juni 21, 2024.
Picha ya majengo yalioharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha China.Picha ya maktaba Juni 21, 2024.

Shirika la habari la serikali ya China, Xinhua limesema kuwa watu sita wamekufa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kusini magharibi mwa China, wakati hali ya joto kali kuliko kawaida ikishuhudiwa kwenye msimu huu wa joto.

Mvua za msimu zilinyesha kwenye kaunti ya Dianjiang, karibu na mji wa Chonqing, kuanzia usiku wa Jumatano hadi leo asubuhi, shirika hilo la habari la Xinhua limeongeza kusema, wakati likinukuu maafisa wa kieneo.

Televisheni ya kitaifa inayomilikiwa na serikali ya CCTV, ikunukuu afisi ya mafuriko ya kaunti, imeripoti kuwa watu wanne wamekufa kutokana na mkasa wa kijeolojia, huku wengine wawili wakisombwa maji mapema leo. Xinhua limeongeza kusema kuwa mmoja wao alikufa kutokana na kuporomoka kwa nyumba, huku watatu wakifunikwa na maporomoko ya ardhi.

Karibu watu 7,000 wameathiriwa na mvua hizo, huku 170 wakiokolewa. Ripoti zimeongeza kusema kuwa hadi milimita 254.6 za mvua zimeshuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo ya Dianjiang, kikiwa kiwango kikubwa zaidi cha kila siku kuwahi kushuhudiwa katika historia ya upimaji.

China inashuhudia joto lisilo la kawaida kwenye msimu huu wa joto, wakati mvua kubwa zikiendelea kunyesha pande za mashariki na kusini, huku sehemu kubwa ya kaskazini ikishuhudia mawimbi ya joto kali. China ndiyo mzalishaji mkubwa sana wa gesi za greenhouse duniani, hali ambayo wanasayansi wanasema imepelekea mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.

Forum

XS
SM
MD
LG