Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 29, 2023 Local time: 12:20

Zanzibar: Wafanyakazi wa Hoteli waitaka serikali kuzipatia ufumbuzi kero zao


Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Fatuma Khamis

Mikataba mifupi ya ajira, unyanyasaji katika sehemu za kazi pamoja na kukosekana kwa chombo maalumu cha kuwasemea wafanyakazi wa hoteli za kitalii, Zanzibar, ni miongoni mwa changamoto wanazopitia wafanyakazi hao na kuwalazimu kuitaka serikali kuwafuatilia wawekezaji wa biashara ya hotel.

Huku serikali ya mapinduzi Zanzibar licha ya kupelekewa malalamiko hayo kwa muda mrefu bado imeendelea kutoa ahadi ya kuzitatua changamoto hizo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Zanzibar, visiwa hivyo viliwapokea watalii 550,000 mwaka 2022 na kuilazimu serikali kuanza kuboresha huduma zinazotolewa na wadau wa utalii. Lakini wafanyakazi wa hotel wanalalamika kuhusu changamoto zinazowakabili na kwamba serikali imeshindwa hadi sasa kuzipatia ufumbuzi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni mikataba mifupi wanayo pewa na ubaguzi katika maeneo ya kazi kuendelea kufanyika hali inayo pelekea kwa upande wao kukosa ufanisi na ufanyaji wa kazi kuzidi kuwa mgumu huku na wao wakitaka wapewe vipaumbele vya ajira kama wanavyopewa wageni na serikali kuwapatia heshima kwakuwa wamekuwa wakichangia katika pato la nchi.

Oscar Mwangiluke miongoni mwa wafanyakazi wa hoteli visiwani Zanzibar anasema: "Mikataba yetu ni miezi sita au mwaka pili unyanyasaji unao endelea kwenye hizi hoteli unakuta mzawa hapewi kipaumbele cha ajira lakini asiekuwa mzawa ndie anaepewa kipaumbele cha ajira na hakuna chombo chochote ambacho kimewahi kutusemea au kutujulia hali na maendeleo sisi ya wafanyakazi labda serikali kutudai kodi na kadhalika."

Malalamiko mengine yaliotolewa na wafanyakazi wa kike ni pamoja na kupewa masharti ya kufanya ngono na waajiri wao au wageni sambamba na kufanyishwa kazi saa nyingi bila ya malipo ya ziada wakiongezea kuwa licha ya mshahara mdogo wanaopatiwa na kukatwa lakini hoteli hizo zimekuwa hazipeleki michango yao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF)

Talha Othumani akizungumza na sauti ya Amerika ameitaka serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kufuatilia ili wananchi wa Zanzibar wanufaike na uwekezaji huo.

Othumani anaeleza: "Baadhi ya hizo hoteli kuna kitu kinaitwa ZSSF hawapeleki michango ukienda kule ukifuatilia unakuta hamna hata shilingi ilioingia ukirudi huku kuwaambia wanakwambia sisi tumesha peleka serikali isibweteke tu ikasema kwamba imepata wawekezaji wanaingiza lile pato lao, wao wanaingiza pato lao lakini je wananchi wao wanafaidika vipi na hizi kazi kweli wanapata haki zao stahiki ?."

Hata hivyo Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu huko Vuga amekiri kuzitambua changamoto zote ambazo wamekuwa wakizipitia wafanyakazi hao na kuahidi tena serikali kuzifanyia kazi.

Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi
Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi

Mwinyi anaeleza:" Tunajua kuna matatizo ya mikataba ndani ya hoteli tunajua kuna matatizo ya watu kutopata nafasi nzuri bado wanapewa zile za chini tunajua yote hayo lakini yanashughulikiwa na sekta husika,kwahiyo tushughulikie matatizo ya pande zote mbili hilo linafanyiwa kazi."

Wafanyakazi hao wamemuomba Rais wa Zanzibar kukutana nao ili waweze kumfikishia yale yanayo wasumbua kwa muda mrefu kwakuwa nawao wanamchango katika sekta ya utalii visiwani humo hasa katika kipindi hiki cha uchumi wa bluu.

Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG