Rais Weah alisafiri kwenda nchi za nje mwishoni mwa mwezi wa Oktoba kwa mikutano kadha katika mataifa mbali mbali na baadae kwenda Qatar ambako amekua akimtizama kijana wake akichezea timu ya Marekani kwenye Kombe la Dunia.
Tangu wakati huo, kiongozi huyo ambae mwenyewe alikua mchezaji kandanda mashuhuri, hajaonekana nyumbani ambako wananchi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na upungufu wa bidhaa muhimu.
Ingawa watu wanafahamu umuhimu wa diplomasia na kazi za rais nje ya nchi. Lakini picha na video zinazomuonesha Weah akistarehe kwenye viwanja vya michezo vya Qatar, akiwa mgeni wa heshima katika Kombe la Dunia, wakati wananchi wake wanataabika, haikupokelewa vizui na kuzusha hasira nchini na kwenye mitandao ya kijami ya Waliberia.
Mwezi uliyopita Rais Weah aliongeza muda wake wa kubaki nje ya nchi kwa siku 25, ikiwa muda mrefu tangu kua rais na anatazamiwa kurudi Liberia Disemba 18.
Serikali yake inakosolewa vikali kutokana na jinsi inavyoshughulikia zowezi la kuhesabu watu linalobidi kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2023.
Weah aliyeingia madarakani mwaka 2017 aliahidi kupambana na umaskini na ulaji rushwa, amechaguliwa na chama chake kugombania mhula wake wa pili. Lakini wapinzani wake wanasema ameshindwa kutekeleza ahadi zake.
Habari za ripoti hii zimekusanywa kutoka AFP.